UMUHIMU WA MACHO YA KIROHO
UMUHIMU WA MACHO YA KIROHO
Na: Mtumishi Frank Mwakapeta
BWANA YESU asifiwe…
Somo hili limegawanyika katika sehemu zifuatazo;
A. Maana ya macho ya kiroho
B. Faida za macho ya Kiroho
C. Mifano ya watu wenye macho ya kiroho
D. Mifano ya watu wasio macho ya kiroho
E. Madhara ya kukosa macho ya kiroho
F. Mambo ya kufanya ili uwe na macho ya kiroho
A. MAANA YA MACHO YA KIROHO
Kwa ujumla mwanadamu yeyote anaishi sehemu mbili tofauti; ulimwengu wa mwili na ulimwengu wa roho. Ulimwengu wa mwili ni ulimwengu unaoonekana kwa macho ya nyama (haya mawili ya kawaida). Kwa mfano, macho ya nyama yanaweza kuona kiti, nyumba, mti, gari na ardhi pamoja na vitu vingine vinavyoonekana kwa macho ya kawaida.
Ulimwengu wa roho ni ule usioonekana kwa macho ya kawaida. Vitu vya ulimwengu wa roho havionekani kwa macho haya ya kawaida. Kwa mfano, mtu hawezi kumuona mchawi kwa macho ya kawaida, hawezi kuwaona malaika kwa macho ya kawaida. Hawezi kuona nguvu za roho mtakatifu kwa macho ya kawaida.
Kwa mantiki hii mwanadamu anahitaji kuwa na macho yanayoweza kuona vitu visivyoonekana kwa macho haya ya kawaida. Na macho hayo yanaitwa "Macho ya kiroho". Huu ni uwezo wa kiroho wa kuona mambo katika ulimwengu wa roho. Ni uwezo alionao mtu kuona mambo yasiyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida
Neno la Bwana linasema hivi,
"Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza..." (Mathayo 6:22,23).
Neno hili liko wazi. Ni ukweli usiopingika kwamba kama huna macho (huoni) kila kitu kinakuwa giza. Utaona kila utazamalo ni giza. Vivyo hivyo hata kwa mambo ya kiroho, usipokuwa na macho ya kiroho huwezi kuona chochote kinachoendelea katika ulimwengu huo. Wachawi wanaweza wakawa wanachafua chakula chako mezani wala usiweze kuona, maana huna macho ya rohoni.
Laiti kama ungelifunuliwa leo, japo kwa dakika moja tu, ili uone mambo yanayoendelea sasa katika ulimwengu wa roho, ungelishangaa sana tena ugelipigwa na butwaa!!! Kuna mambo mengi usiyoyajua yanaendelea huenda hata muda huu. Yawezekana muda huu hapo ulipo kuna wachawi wako kwenye nyungo wanapita hapo ulipo kuelekea eneo fulani, lakini wewe huwaoni. Kwanini? Ni kwa sababu huna macho ya rohoni hivyo huwezi kuona na ndio maana neno linakutaka umwombe Mungu akupe macho ya rohoni ili uweze kuona mambo makubwa na magumu uliyokuwa huyajui ( Yeremia 33:3).
Uwezo wa kuona kiroho ni kazi ya macho ya rohoni. Kama mtu wa Mungu, macho yako ya kiroho yanapaswa kuona kwa maana Roho mtakatifu yupo ndani yako yeye achunguzaye mambo yote hata mafumbo ya Mungu. Biblia kwenye 1 Wakorintho 2:10 imeandikwa hivi,
"Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu"
Hivyo utagundua kwamba kazi ya kuona kiroho si kazi ya nabii, bali ni kazi ya Roho mtakatifu. Sasa kama wewe una roho mtakatifu unatakiwa uwe na uwezo wa kuona kila kitu. Kama Roho mtakatifu anaweza kujua kila kitu hadi mafumbo ya Mungu, kwanini wewe ushindwe kuona ikiwa Roho aliye ndani yako ana uwezo mkubwa kiasi cha kutambua hata mafumbo ya Mungu?
B. FAIDA ZA MACHO YA KIROHO
1. Yatakusaidia kuwatambua watumishi wa uongo na wale wa kweli.
Ni vigumu sana kujua nani ni mtumishi wa Mungu wa kweli na yupi ni wa uongo, hususani katika kipindi hiki ambacho kuna ongezeko kubwa la watumishi wa uongo, wanaohubiri kwa kutumia nguvu za giza. Ongea yao, tembea yao ja kuvaa kwao ni kama watumishi wa kweli lakini kumbe ndani ni waongo. Mtu asipokuwa na macho ya kiroho atajikuta anaabudu kwa miungu mingine. Yesu katika kitabu cha Mathayo 7:15 anasema,
"Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali".
Watu wengi siku hizi wamepotoshwa, wametabiriwa unabii wa uongo lakini bado wao wanaamini kuwa hao ni watumishi wa kweli. Nani atakayewaambia kuwa hao sio watumishi wa kweli kama hawatakuwa na macho ya kiroho? Macho ya kiroho ndiyo yatakayokusaidia kujua ni mtumishi yupi ana Mungu wa kweli, ni kanisa gani lina Mungu wa kweli. Bila hivyo, mtu atapotea kabisa.
2. Yatakusaidia kujikosoa, kujirekebisha na kubadilika kiroho
Ni rahisi sana kwa mtu kuwanyooshea wengine vidole kuwaona wana dhambi, lakini ni vigumu sana kujitambua yeye mwenyewe kwamba ni mkosaji mbele za Mungu. Ni macho ya kiroho tu yatakayomsaidia mtu kuona uovu wake mwenyewe na ndiposa ataweza kubadilika. Pasipokuwa na macho ya kiroho mtu atajiona yeye ana haki muda wote na kuona wengine ndio wana dhambi au ubaya, lakini kumbe yeye pia ana kasoro ila tu hajaona kwakuwa hana macho ya rohoni. Sharti aondoe kwanza giza kwenye macho yake ndipo aanze kukosoa/kusaidia wengine. Ndicho Yesu anachokisema hapa, anasema;
"Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako. (Mathayo 7:4,5)
3. Yatakufanya uweze kuwasaidia wengine (humsaidia kiongozi kuwajua watu wake)
Huwezi kumuongoza kipofu ikiwa na wewe ni kipofu. Ukitibu macho yako ndipo sasa utaweza kuwasaidia vipofu wengine. Mtumishi ye yote asiye na macho ya rohoni, iwe ni mchungaji, mzee wa kanisa, kiongozi wa kwaya au kundi lolote lile; hawezi kuwasaidia waumini wake kiroho kwa sababu atashindwa kuona madhaifu yao. Lakini mtumishi aliye na macho ya kiroho ataona uasherati ndani ya waumini wake na ataukemea.
Siku moja Yesu aliwafokea Mafarisayo (viongozi wa dini) akawaambia "mnaniheshimu kwa midomo tu lakini mioyoni mwenu hamniheshimu". Aliposema maneno hayo, Kumbe! Mafarisayo wakawa wamechukizwa sana."Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? Akajibu, akasema,......Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili" (Mathayo 15:12-14)
Unaona madhara ya kuongoza watu na huku wewe mwenyewe ni kipofu? Wote mtaangamia. Wapo waumini ambao kwa macho ya kawaida wanaonekana wanafaa sana kuwepo kanisani, lakini kumbe ni wachawi, walevi, malaya n.k. Na mchungaji wao asipokuwa na macho ya rohoni, anaweza kuwachagua hao kuwa wapishi wa kanisa, wazee wa kanisa, waongoza sifa au hata kuwapa nafasi ya kuhubiri ibadani. Laiti angekuwa na macho ya rohoni, angeweza kuwaita na kukemea dhambi zao.
4. Yatakufanya usitende dhambi
Wapo watu wengi ambao wamehalalisha dhambi fulani kuona ni jambo la kawaida, na hata ukiwashauri watakuambia hili ni jambo la kawaida wala sio dhambi. Kwa mfano, kuna watu wanadhani matusi sio dhambi, kwahiyo wao hutukana hovyo tu. Yote haya ni kwasababu hawana macho ya rohoni yenye uwezo wa kuona madhara ya matusi katika ulimwengu wa roho. Lakini kwa mtu aliye na macho ya rohoni atajua lipi jema na lipi sio jema. Kabla hajalitenda baya ataweza kuona madhara yake na hivyo ataacha asilifanye.
5. Yatakufanya ufanane na Yesu (na Mungu)
Yesu alikuwa na uwezo mkubwa wa kuona mambo yasiyoonekana. Na kilichomsaidia Yesu kwenye huduma yake ni macho ya rohoni. Aliweza kujua mahitaji ya watu hata bila kuambiwa. Alijua hila na nia mbaya ya Mafarisayo dhidi yake hata bila kuambiwa. Kuna wakati alikuwa akiona hatari mbele zake alikuwa anaagiza kuondoka ili waende eneo lingine tofauti. Macho ya kiroho ndiyo siri ya ushindi wa Yesu Kristo. Na wewe ukitaka uwe mshindi kama Yesu tafuta sana kuwa na macho ya kiroho.
6. Yatakusaidia kuwatambua wabaya wako
7. Yatakusaidia kuchagua marafiki sahihi.
C. MIFANO YA WATU WENYE MACHO YA KIROHO
1. MUNGU MWENYEWE ANA MACHO YA ROHONI
Biblia imeandikwa hivi; Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba (Mwanzo 1:27). Kwa mstari huu tunapata kujua kwamba sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Kama yeye alivyo ndivyo na sisi tulivyo. Alicho nacho nasi tunapaswa kuwa nacho. Mungu anayo macho ya kiroho. Biblia imeandikwa hivi;
"Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana......Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.......Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa (Zaburi 139:1-4, 7, 8, 11, 12).
Katika mistari hii tunaona uwezo mkubwa wa Mungu wa kuona mbali sana. Huo sio uwezo wa macho haya ya kawaida. Ni macho ya kiroho. Uwezo wa kuona mawazo ya mtu, maneno ya ulimi wa mtu, kuona hadi kuzimu na kuona hata gizani, sio wa macho ya kawaida bali ya rohoni. Sasa tukirudi kwenye mstari wa Mwanzo 1:27 ni lazima tumuombe atupe uwezo wa kuona rohoni kama yeye; maana amesema mwenyewe kwamba ametuumba kwa mfano wake.
Wapo watu kwenye Biblia ambao walikuwa na macho ya kiroho na tunaona jinsi yalivyowasaidia. Pia wapo ambao hawakuwa na macho ya kiroho na tunapata kuambiwa jinsi walivyosumbuka kutokana na kukosa macho hayo ya kiroho. Hebu tuwaangalie:
2. YESU ANA MACHO YA ROHONI
Kama Yesu asingekuwa na macho ya rohoni hakika angepata tabu sana kutenda kazi aliyojia humu duniani. Asingeweza kuwatambua watu wenye hila na wabaya wake. Lakini yeye alikuwa na macho ya kiroho. Alikuwa na uwezo wa kuona yaliyofichwa. Angalia visa vifuatavyo:
a). Aliona mawazo ya Nathanaeli (Yohana 1:47-49)
Siku moja Filipo alikuwa anamueleza Nathanaeli ya kwamba ameonana na Yesu. Lakini Nathanaeli akawa haamini. Hivyo Filipo akamchukua Nathanaeli mpaka kwa Yesu ili amuone aweze kuamini. Yesu alipomuona Nathanaeli, akasema ".....tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake" (Yohana 1:47).
Mpendwa msomaji hebu jaribu kufikiria ni kwa namna gani Yesu aliweza kutazama hadi ndani ya mwili (mawazo) wa Nathanaeli. Je, aliwezaje kuona kwamba ndani ya Nathanaeli hamna hila? Hata Nathanaeli mwenyewe alishangaa sana. Ndiyo maana mstari wa 48 Nathanaeli akauliza akisema; "......Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.
Tunachojifunza hapa ni kwamba macho ya rohoni ni muhimu sana maana yatakusaidia kuwabaini maadui au marafiki. Wangali wako mbali utaweza kujua kuwa huyu amekuja kwa nia mbaya.
b). Yesu aliyajua mawazo ya waandishi (Mathayo 9:1-4)
Siku moja walimletea mtu aliyepooza naye akamponya na kumwambia ainuke aende. Akiwa anafanya hivyo palikuwepo na watu kando yake wakawa wanajisemesha nafsini mwao wakisema "Huyu anakufuru". Katika hali ya kawaida haiwezekani kuona kitu anachokiwaza mtu, hususan kama hajakisema kwa sauti. Hapa tunaambiwa watu hawa walikuwa wanajisemea nafsini mwao, sio kwa sauti. Ajabu ni kwamba licha ya wao kujisemesha mioyoni mwao, bado Yesu aliyaona mawazo yao, akawaambia akasema; "Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu?" (Mathayo 9:4).
Ndugu yangu, hebu tamani kumuomba Mungu akupe macho ya kiroho. Ukiwa nayo utaweza kujua mawazo mabaya wanayokuwazia watu. Kuna watu wanaweza wakawa wanacheka na wewe, wanakukumbatia kabisa, lakini kumbe mioyoni mwao wanawaza ufe papohapo. Ukiwa na macho ya Kiroho kama Yesu utaweza kutambua hila zao na utaweza kuwashinda.
c) Yesu aliuona uhai ndani ya mtu aliyedhaniwa kuwa amekufa (Mathayo 9:24-26)
Mtu mmoja (jumbe) alimfuata Yesu akiwa anafundisha watu, akamwambia binti yake amekufa na akawa anamuomba aende nyumbani kwake akamuwekee mikono akiamini kwa mikono ya Yesu mtoto wake angefufuka. Yesu alikubali akaenda mpaka nyumbani kwa yule jumbe. Akamkuta binti amelala na watu wanaomboleza. Yesu alipomuangalia yule binti akagundua kwamba hakufa bali alikuwa hai. Akawaambia wale waombolezaji "Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana (Mathayo 9:24)
Angalia, wao wanamcheka wakidhani yule mtoto amekufa lakini kumbe hajafa. Hawakuwa na macho ya kiroho kuweza kuona kuwa bado kuna uhai ndani ya binti. Yesu kwa kutumia macho ya rohoni aliona kwamba bado binti yu hai. Alipoingia ndani akamwita yule binti na kweli akafufuka. Yesu aliwahi kufanya jambo kama hili siku alipomfufua Lazaro. Hata huko nako watu hawakuamini lakini yeye alipotazama kwa macho ya kiroho aliona Lazaro hakufa (Yohana 14:1-44).
Hebu jiulize, kwa namna hii jinsi ambavyo wengi wetu hatuna macho ya rohoni, ni wangapi tumewazika wangali hai? Yawezekana tunasema kabisa "BWANA ametwaa" lakini kumbe wala hajafa ila amechukuliwa msukule anafanya kazi kwenye shamba la mtu. Huku tunasema amekufa kumbe hapana. Lakini tungekuwa na macho ya rohoni tungeweza kutambua kuwa mtu hajafa.
Kuna mambo mengi tumeyaacha tukidhani yamekufa kumbe hapana. Ukiwa na macho ya kiroho hutakata tamaa haraka. Unashangaa biashara au shughuli ileile ambayo wewe unataka kuacha ndiyo hiyo mwenzako anataka kuanzisha mahali palepale ulipo wewe. Mwenzako anaona kwamba baada ya miezi sita biashara/shughuli hiyo itamtoa kimaisha. Wewe unaamua kuacha kwa sababu huna macho ya kiroho ya kuona mbali mafanikio yatakayokuja baada ya miezi sita.
d). Yesu aliweza kutambua kuwa Petro angemkana mara tatu.
Hapa kuna kitu cha ajabu sana. Yaani Yesu alijua mpaka idadi kwamba Petro angemkana mara ngapi. Wakati Petro anajitutumua akisema kwamba angekufa na Yesu, Yesu akaanza kumchunguza Petro kwa macho ya kiroho na akaona kwamba usiku uleule angemkana mara tatu. Yesu akamwambia,
"....Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu" (Mathayo 26:34)
Wakati Yesu anasema haya Petro mwenyewe alikuwa hajui kama kweli hayo yangetokea baadaye. Ajabu ni kwamba ni kweli baadaye Petro alimkana Yesu mara tatu vilevile alivyosema Yesu. Mafarisayo walipomuuliza kama naye ni mfuasi wa Yesu, alikataa. Akaulizwa tena mara ya pili akakataa. Mara ya tatu "Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo (Mathayo 26:74)
Mpendwa msomaji, Yesu anasema hivi; "Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya......" (Yohana 14:12). Kwa ahadi hii tunapaswa kuwa na macho ya rohoni maana yeye alikuwa nayo. Kama yeye aliweza kuona hata mawazo ya ndani ya mtu, sisi nasi tunapaswa kuwa na uwezo huo na ikiwezekana sisi tuone makubwa zaidi ya hayo maana anasema tukimwamini tunaweza kufanya zaidi yake. Kwa lugha nzuri tunaweza kusema yeye aliona kwa kiwango kidogo sisi tunatakiwa tuone zaidi ya pale alipoishia.
3. ELISHA ALIKUWA NA MACHO YA KIROHO
(a). Alimtambua mtu aliyetumwa kumuua kabla mtu huyo hajafika (2Falme 6:24-33)
Ben-hadadi mfalme wa Shamu aliivamia Samaria iliyoko Israeli. Basi kukawa na njaa sana huko Israeli, hali iliyopelekea watu kuwala watoto wao. Wanawake wawili walipatana kuwala watoto wao. Mmoja wao baada ya kula mtoto wa mwenzake akamficha wa kwake. Ndipo yule aliyedhulumiwa akaenda kushitaki kwa mfalme wa Israeli. Na mfalme aliposikia habari ya kula watoto alirarua nguo zake. Kisha akaahidi kumuua Elisha (maana aliamini kwamba njaa ile imetokana na Elisha, kwani ndiye nabii anayeweza kuomba jambo na likatokea). Ndipo mfalme akamtuma mtu aende kwa Elisha kumuua.
"Lakini Elisha alikuwa akikaa nyumbani mwake, na wazee wakikaa pamoja naye; na mfalme akamtuma mtu wa mbele yake; lakini hata kabla ya kufika kwake yule aliyetumwa, akawaambia wazee, Je! Mwaona jinsi huyu mwana wa mwuaji alivyotuma aniondolee kichwa changu? Angalieni, huyo aliyetumwa akifika, fungeni mlango, mkamzuie mlangoni; je! Sauti ya miguu ya bwana wake haiko nyuma yake? (2Falme 6:32)
Mpendwa msomaji, mstari wa hapo juu utashangaa sana. Yaani Elisha yuko nyumbani kwake lakini tayari amejua kwamba mfalme wa Israeli katuma mtu wa kumuua. Kumbe usipokuwa na macho ya rohoni uwezekano wa kufa mapema ni mkubwa maana hutaweza kuona adui anapokujia.
(b). Alikuwa na uwezo hata wa kuyaona mawazo ya mtu.
Katika kipindi cha Elisha, kulikuwa na mfalme wa Shamu alipanga vita dhidi ya Waisraeli mara nyingi lakini hata hivyo hakufanikiwa kuwapata kwa maana kila alipokuwa akipanga,Waisraeli walijua mara moja na kuwawahi maadui zake. Siku moja mfalme wa Shamu alighadhibika na kuwauliza watumishi wake,“ Ni mtu yupi miongoni mwetu aliye upande wa mfalme wa Israeli ? ” ( kwa maana alifikiri labda kuna mtumishi wake mmoja wapo aliyekuwa akivujisha taarifa zake).
Lakini "Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala (2Falme 6:12)".
Unaona? Yeye alidhani kuna mtu anavujisha siri, lakini wakamwambia sivyo mfalme, bali kuna mtu anaitwa Elisha, yeye ni nabii wa Israeli anayejua hata mambo yako unayoyapanga kwenye chumba chako cha kulala. Uwezo huu wa kuona mambo ya chumbani kwa mtu sio wa kawaida; ni mpaka uwe na macho ya rohoni.
4. KALEBU ALIKUWA NA MACHO YA KIROHO
Biblia inasema "Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli;....." (Hesabu 13:1)
Miongoni mwa watu 12 waliochaguliwa na Musa kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani alikuwemo Kalebu. Basi wakaenda wakaipeleleza nchi na wakagundua ni nchi nzuri, yenye matunda ya kutosha. Walichuma baadhi ya matunda na wakarudi kwa Musa kumpa taarifa ya upelelezi walioufanya kwa siku arobaini (Hesabu 13:23-26)
"Wakamwambia wakasema, tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. LAKINI watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko" (Hesabu 13:27-28)
Mpendwa msomaji, neno "LAKINI" linaharibu uzuri wote waliouona kwenye ile nchi. Wanasema nchi ile ni nzuri, LAKINI ina watu wa kutisha (hodari) kuliko wao. Maneno haya ni maneno ya kuwakatisha tamaa wapokea taarifa.
Jambo la ajabu ni kwamba, Kalebu alikuwa na mtazamo tofauti na wenzake. Wakati wenzake wanaogopa wale watu hodari na maboma makubwa, yeye aliiona kuwa ni nchi nzuri sana inayofaa kuishi. Hakuona chngamoto ndani yake. Ndipo Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka (Hesabu 13:30). Yaani macho ya wenzake yaliona kama nchi ile haifai kukaliwa kwakuwa ina watu hodari (wenye nguvu) kuliko wao, lakini macho ya Kalebu yaliona mbali zaidi. Yaliona uwezekano wa kuwashinda wale watu hodari.
Kalebu akasema, Jamani! Mbona mimi nikiwaangalia wale wa Anaki naona kama tunaweza kuwashinda kabisa? Lakini wao, kwa sababu ya kutokuwa na macho ya kiroho yenye kuona mbali zaidi, wakasema hatuwezi kwenda kupigana nao maana wana nguvu kuliko sisi, tena ile nchi inakula watu; na sisi ni kama mapanzi tu kwa wale Wanefili [wana wa Anaki] (Hesabu 13:30-33).
Unaona sasa? Wale wenzake, kwa macho haya ya kawaida walijiona ni dhaifu kama mapanzi, na kwamba kama wangeenda kule wangeuawa, wangeliwa, wangepigwa. Lakini Kalebu kwa macho ya kiroho akaona zaidi ya walivyoona wenzake. Yeye aliona ushindi, aliona kufanikiwa ndani ya nchi ileile ambayo wengine wanaona kifo. Lakini watu, kwa sababu ya kutiwa hofu na wale wasio na macho ya kiroho wakazidi kusema bora wangerudi Misri kuliko kwenda kufa kule Kanaani.
Yoshua na Kalebu (wapelelezi wenye macho ya kiroho) wakajaribu kusema na makutano wakisema; Jamani, sisi tunaona ile nchi ni nzuri sana. Kama Mungu akitupa kukaa mule, tutakuwa tumebahatika sana. Jamani, mna shida gani? Kwanini ninyi mnaona kifo na kushindwa wakati sisi tunaona maziwa na asali huko? (Hesabu 13:6-8).
Mungu alipoona watu wanazidi kukataa kwenda Kanaani kwa hofu ya yale majitu makubwa (wanefili), alikasirika akasema hakika watu hawa watakufa. Musa akajaribu kuwaombea msahama. "BWANA akasema, nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa; lakini....hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao.....LAKINI MTUMISHI WANGU KALEBU KWAKUWA ALIKUWA NA ROHO NYINGINE NDANI YAKE.....nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia, na uzao wake watamiliki" (Hesabu 14:20-24).
Mpendwa msomaji, Mungu anasema ndani ya Kalebu mlikuwa na roho nyingine iliyomsaidia kuona vizuri yale ambayo wengine hawakuweza kuyaona. Unadhani ni roho gani hiyo? Ni Roho mtakatifu; huyo akikaa ndani ya mtu, atamsaidia kuwa na macho ya kiroho kwa sababu yeye mwenyewe ni Roho. Roho mtakatifu anatenda mambo yake kiroho, kwahiyo anaweza kumpa mtu uweza wa kuona mambo ya kiroho, ambayo wengine hawawezi kuona. Huna budi kumuomba Mungu akupe roho mtakatifu akae ndani yako ili uweze kuwa na macho ya kiroho na uweze kuona yale ambayo watu wengine hawaoni.
Tunachojifunza kwa Kalebu;
1. Usipokuwa na macho ya Kiroho unaweza kumkosea Mungu. Kwa sababu utashindwa kuenenda atakavyo yeye. Anaweza akawa anakuonesha fursa ili ufanikiwe lakini kwakuwa huna macho ya kiroho, huoni, utabaki kuwa maskini. Ataona kama una kiburi. Anakwambia usimuoe fulani, lakini kwakuwa huna macho ya rohoni kuona kasoro za huyo msichana utaoa tu. Tayari Mungu atakukasirikia kuona kama una kiburi. Tumeona hapa kwamba Mungu anawaambia wana Israeli wahamie Kanaani kwakuwa ameona ni nchi nzuri kwao, lakini wao kwa sababu ya kukosa macho ya kiroho wanapingana naye wanasema nchi ya Kanaani ina majitu, inaua watu.
2. Wengi wameshindwa kufanikiwa kimaisha kwa sababu hawana macho ya kiroho. Wanashindwa kuona fursa zinazowazunguka. Ndio maana unakuta anakuja mtu toka mbali ananunua eneo hulo kwenu anajenga duka au ofisi ama anaandaa shamba na kufanikiwa sana. Wewe mwenyeji, unabaki unashangaa tu; Hee! Jamani ningejua nami ningekuwa nimenunua eneo hili, ningetoboa maisha. Awali hukunua kwa sababu uliona ni eneo la kawaida lisilo na faida. Lakini wenye macho ya kiroho wameona eneo hilo litawatoa kimaisha. Kalebu mwenye macho aliona ardhi ya Kanaani inafaa, lakini wasio na macho ya kiroho wakaona haifai
D. MIFANO YA WATU WASIO NA MACHO YA KIROHO
1. GEHAZI, MTUMISHI WA ELISHA ALIKOSA MACHO YA KIROHO
Baada ya Mfalme wa Shamu kuambiwa kwamba Elisha ndiye anayevujisha siri zake kwa mfalme wa Israeli, akakusanya kikosi cha wanajeshi waende kwa Elisha ili kumkamata. Mtumishi wa Elisha (Gehazi) alipoyaona majeshi ya Shamu, aliogopa sana, akakimbia kwenda kumwambia bosi wake akisema; "Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?"(2Falme 6:15).
Unajua kwanini anaogopa? Ni kwa sababu anaona jeshi la maadui ni kubwa mno, hawawezi kushindana nao. Lakini Elisha; “Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao."(2Falme 6:16).
Elisha alipotazama jeshi la Washami wala hakuogopa maana kwa macho ya rohoni aliona kwamba walio upande wake (jeshi la Mungu) ni wengi kuliko jeshi la adui zake. Lakini Gehazi hakuweza kuona jeshi la Mungu lililokuwa upande wake. Kwanini? Ni kwa sababu macho yake ya rohoni yalipofushwa na shetani.
Ndipo "Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.“ (2 Wafalme 6:16-17).
Ninaamini kwamba baada ya kuombewa na Elisha, macho yake ya rohoni yalipoona hakuogopa tena. Tunajifunza jambo, kwamba ikiwa huwezi kuona kiroho ni rahisi kumwogopa adui yako, kwa maana macho ya damu na nyama huleta hofu/ hudanganya. Ndiyo maana watu wanaogopa bundi, Paka, wachawi. Lakini ikiwa utafanikiwa kumwona adui yako kiroho, na jinsi nguvu ya Mungu iliyopo upande wako ilivyo kubwa, huwezi kumkimbia adui yako au kumwogopa.
Unafikiri kwa nini Elisha hakuweza kuteteleka/hakuogopa? Kwa sababu alikuwa akiona kiroho na kuyaona majeshi ya Shamu ni madogo sana yenye kiwango cha chini ukilinganisha na majeshi ya Bwana. Bila shaka, Elisha alipewa uwezo wa kuona kiroho. Alipowatazama hakuona chochote cha kumtisha. Hutakiwi kuogopa adui zako. Ipo nguvu ya Mungu kubwa zaidi ya nguvu ya adui, iliyokuzunguka. Pia tunajifunza kwamba unaweza ukawa mtumishi uliyekosa macho ya rohoni kama mtumishi wake Elisha; ama unaweza ukawa mtumishi mwenye macho ya rohoni, kama Elisha alivyokuwa.
Pia Macho ya rohoni yanaweza kufumbuliwa, na hatimaye ukaona kiroho. Elisha alipomwomba Mungu kwa habari ya kufunguliwa macho ya mtumishi wake, hakika Bwana alitenda kwa kumfungua macho ya rohoni naye akaona. Na ndivyo ilivyo hata wakati huu, ukiwa huwezi kuona kiroho, muombe Mungu akufumbue macho yako yaweze kuona.
2. KLEOPA NA MWENZAKE HAWAKUWA NA MACHO YA KIROHO
Habari zao zinapatikana kitabu cha Luka 24:13-45. Tunaambiwa kwamba siku ambayo akina Magdalena walienda kaburini na kukuta Yesu hayumo kaburini, Kleopa na mwenzake wakawa wanatembea kwenda kijiji cha Emau. Wakiwa njiani wakawa wanajadili habari za kifo cha Yesu. Katika kujadili ghafula Yesu akajiunga nao lakini wao hawakujua kama ndiye Yesu mwenyewe. Unajua kwanini hawakumtambua? Ni kwa sababu macho yao ya rohoni yalikuwa yamefumbwa. Wanamuona kabisa lakini hawajui kuwa ni Yesu wanayemjadili. Biblia inasema "Macho yao yakafumbwa wasimtambue (Luka 24:16).
Basi Yesu akajifanya kama siye yeye; akawauliza "jamani mnajadili habari gani"? Wakamjibu (nadhani kwa hasira) wakasema " ina maana wewe ni mgeni eneo hili? Unauliza kwani hujui kilichomtokea Yesu mnazareti, kwamba wakuu wetu wamemhukumu na kumuua, mtu tuliyemtumaini"?. Ingekuwa ni vijana wa kipindi hiki huenda wangemjibu, "we vipi? Acha kutuzingua bwana, unajifanya hujui kinachoendelea?
Mpendwa msomaji, unaona wanavyomjibu? Yaani wanaeleza kuonesha kwamba walimjua Yesu vizuri sana. Lakini ajabu ni kwamba hawakujua kuwa anayewauliza ndiye Yesu mwenyewe, wanayejifanya kama wanamjua sana. Upofu wa macho ya kiroho ni zaidi ya ugonjwa. Bila macho haya huwezi kuujua ukweli. Biblia inasema aliendelea nao mbele huku anajadili nao. Akawa anajaribu kuwapa hata mistari ya maandiko inayoonesha kuwa suala la Yesu (yeye) kufa lilikwisha kuandikwa kuwa lazima litimie (Luka 24:25-27).
Pamoja na hayo bado wakawa hawajui kuwa ni yeye anaongea nao. Wakafika Emau bado wakawa hawamtambui, ni mpaka alipokaa na kula nao mezani ndipo Biblia inasema "Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao (mstari wa 31).
Umeona hapa? Wametembea naye njiani mwendo mrefu lakini hawamjui kuwa ndiye Yesu mwenyewe. Baada ya kufumbuliwa macho yao ya rohoni ndipo wanatambua kuwa walikuwa wameongozana na Yesu mwenyewe. Ukisoma mstari wa 45 utagundua kwamba wakiwa njiani hawakuelewa maandiko aliyokuwa anawafunulia kwa sababu macho yao ya rohoni yalifumbwa. Lakini alipowafumbua macho wakaelewa maandiko. Biblia inasema; "Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko (Luka 24:45).
Hivi ndivyo inavyokuwa hata kwetu tusipokuwa na macho ya rohoni. Unaweza kumwacha mchumba mzuri kwa sababu huna macho ya rohoni. Huwezi kuona tabia njema zilizo ndani yake, wewe utaona kuwa hafai. Bila macho ya kiroho utamfukuza mtu atoke kwako lakini kumbe huyo ndiye mlango wa kufanikiwa kwako. Utaidharau fursa fulani kumbe ndiyo ya kukutoa kimaisha lakini wewe utaiona haifai. Siku ukifumbuliwa macho ndipo utaanza kujutia kwamba "jamani ningejua".
E. MADHARA YA KUTOKUWA NA MACHO YA KIROHO
1. Wachawi watakuchezea. Watachafua chakula chako maana huwaoni. Watakulaza uvunguni maana huwaoni wanapokujia
2. Utakuwa na marafiki wasio sahihi, maana hutaweza kutambua mtu sahihi na asiye sahihi
3. Muda wote utakuwa na hofu maishani mwako. Hofu ya maadui, hofu ya kufanya biashara, hofu ya kuanzisha mradi
4. BILA MACHO YA KIROHO MTU HAWEZI KULIELEWA NENO LA MUNGU
Shetani anajua faida apatazo mtu kwa kusoma neno la Mungu. Kwahiyo anachofanya ni KUPOFUSHA MACHO YA KIROHO ya mtu ili asione wala kuelewa neno hilo. Kuna wakati unaweza ukawa unajisomea neno la Mungu halafu ukajikuta hulielewi. Hapo cha kufanya kabla hujatamani kumwita mtu akueleweshe, muombe kwanza Roho mtakatifu akufungue macho yako ya rohoni upate kuona ujumbe uliofichwa ndani ya andiko hilo.
Mara nyingine utamsikia mtu akisema "mimi huwa mhubiri fulani simuelewi kabisa ila fulani namuelewa. Hapo usidhani yule mhubiri hajui kuhubiri ama kufundisha, hapana. Anajua sana tu, lakini kilichokosekana ni macho ya kiroho kwa yule msikilizaji, hawezi kufuatana na ufafanuzi ambao mhubiri anautoa.
Unaposoma neno unasoma maagizo au sheria ya Mungu. Na kama unasoma sheria za Mungu maana yake ukizishika na kuzielewa huwezi kutenda dhambi. Biblia inasema "Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana (Zaburi 119:1).
Unadhani kwa nini inawasifia na kuwapongeza wanaosoma neno (sheria) za Mungu? Ni kwa sababau; Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima (Zaburi 19:7). Kumbe mtu akifuata neno la Mungu anaondolewa ujunga na anakuwa mkamilifu.
Shetani kwa kujua hilo hayuko tayari kumwacha mtu salama. Yeye anataka mtu aharibikiwe maisha, kwahiyo anafanya juu jini kutaka mtu asielewe neno la Mungu maana anajua fika kwamba, mtu akilielewa neno la Mungu kamwe hawezi kuwa mjinga na hawezi kutenda dhambi. Anachokifanya yeye ni KUPOFUSHA MACHO YA KIROHO ya mtu huyo ili ashindwe kuelewa neno.
ZABURI 119:18-19
Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako.
Angalia mwimba zaburi huyu anachomuomba Mungu. Anaomba Mungu amfumbue macho (ya kiroho) ili aweze kuona maajabu yaliyomo kwenye neno (sheria) la Mungu. Kuna maajabu ya Mungu aliyoyaweka kwenye neno lake. Twaweza kusema kwenye neno kuna furushi kubwa la mambo mazuri ambayo Mungu ameweka kwa ajili yetu, mfano; mafanikio, baraka, uponyaji, watoto na mengine mengi.
Lakini haya mambo hayawezi kuonekana bila kutumia macho ya kiroho. Na kwa sababu shetani hapendi mtu ayaone hayo, anachofanya ni kupofusha (kuziba) macho ya kiroho. Kwahiyo mtu anabaki kama alivyo, haoni mabadiliko. Anamuondolea mtu hamu ya kusoma neno. Na hata akisoma bado hawezi kuelewa maana macho ya rohoni yamezibwa.
YOHANA 12:40
Siku moja Yesu alikuwa akiwaeleza makutano kwamba si muda mrefu mwana wa Adamu (yaani yeye mwenyewe) atapaa kwenda juu. Pamoja na kuwafundisha kwa muda mrefu lakini bado hawakumjua nani ni mwana wa Adamu. Wanamuuliza "mwana wa Adamu ni nani"? (Yohana 12:23,34). Hatukutegemea kama watu aliokaa nao kwa muda mrefu wangeshindwa kujua kwamba anaitwa mwana wa Adamu.
Lakini kupitia mstari wa 40 tunapata kujua kilichowazuia washindwe kumjua Yesu. Kumbe ni shetani alipofusha macho yao na ufahamu wao. Mstari huo unasema; "Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya (Yohana 12:40).
Aisee! Unaona hapa? Yaani kumbe shetani ndiye aliyewapofusha macho ya rohoni ili wasimuelewe Yesu eti kwa sababu wangemwelewa wangeponywa na kuongoka (kuacha mabaya na kufuata mema). Kwahiyo, licha ya Yesu kuhubiri kwa muda mrefu wao wakaona kama haeleweki. Walishindwa hata kuelewa mwana wa Adamu ni nani. Ndugu msomaji, usipokuwa na macho ya kiroho huwezi kuelewa mafundisho.
5. UKIONA MTU ANAKATAA KUOKOKA UJUE HANA MACHO YA ROHONI
Unapoona wahubiri wanahubiri halafu watu wanakataa kuokoka ujue watu hao wamepofushwa macho yao wasione raha iliyoko kwenye wokovu. Paulo amehubiri makanisa na maeneo mbalimbali. Alipofika kwa Waefeso aliamua kuwapa wosia (sasa sijui kama walikuwepo waliokataa kuoka). Mtume Paulo anawaambia Waefeso akisema;
"macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa;......(Efeso 1:18-22)
Kwenye mistari hii tunaona kwamba macho ya rohoni ya mtu yakipofushwa hawezi kuona faida ya kumkubali na kumfuata Yesu (kuokoka).
Aliye na macho anaona kwamba akiokoka anakuwa amejipatia tumaini la kudumu ndani ya Yesu, lakini asiye na macho haoni jambo hilo.
Aliye na macho ya rohoni anaona kwamba kuokoka ni utajiri tosha maana anafanyika mrithi pamoja na Yesu kwenye ufalme wa mbinguni, lakini asiye na macho hawezi kuona uzuri huu unaopatikana kwa kuokoka
Mwenye macho ataona kwamba akiokoka anapata uweza wa ajabu ndani ya Yesu wa kufanya makubwa yasiyowezekana katika hali ya kawaida, lakini asiye na macho hawezi kuona zuri lolote ndani ya wokovu.
Aliye na macho ya rohoni ataona kwamba kuokoka ni kujisogeza karibu na Yesu mwenye jina lenye uwezo kupita majina yote, jina lenye kukomesha magonjwa na shida. Lakini kwa aliyepofushwa macho yeye hawezi kuona mazuri haya yaliyo ndani ya wokovu. Yeye ataona kama kuokoka ni kupoteza wakati
Kwahiyo kabla ya kuwaalika watu kuja kuokoka kinachohitajika ni kwanza kuwaombea macho yao ya rohoni yafumbuliwe ili sasa waweze kuona mazuri yaliyomo ndani ya wokovu. Maana asipoyaona hayo hawezi kuvutiwa na wokovu. Baada ya macho yao kufumbuliwa itakuwa rahisi tu kuwaita wapite mbele kuokoka. Watakuja tu.
2WAKORINTHO 4:3,4
Paulo na wenzake walikuwa wamehubiri sana kiasi cha kusema kila mtu angeelewa neno la Mungu. Kwa injili ile hawakutegemea tena kuona mtu asiyemwamini Yesu. Ninaamini Paulo na wenzake walisemezana wakisema; "hee jamani kweli kwa injili hii tuliyopiga eti tusikie mtu anasema hajaielewa, ah! Atakuwa ana shida! Wazo hili likampa Paulo hamu ya kuwaambia makutano, akasema;
"Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu". (2Wakorintho 4:3,4)
Kusitirika ni kufichika (kutokuonekana ama kutokueleweka). Paulo anawaambia watu, jamani ee.. tumehubiri sana kwenu na kama kuna mtu hajaelewa injili yetu huyo sio bure, ufahamu (fikira) wake utakuwa umepofushwa na mungu wa dunia (shetani). Paulo anaongeza anasema; lengo la shetani kuwapofusha ufahamu ni ili msiione nuru (uzuri) ya injili tunayoihubiri.
Mpendwa msomaji, angalia jinsi shetani anavyopofusha macho na ufahamu wa watu kiasi kwamba wanapohubiriwa wanaona kama mahubiri si kitu. Na lengo lake ni ili watu wasiuone uzuri ulio kwenye injili. Kwahiyo mtu anaweza akahubiri sana lakini hakuna anayepita mbele kuokoka, ni kwa sababu shetani amewapofusha macho wasione uzuri/faida ya kuokoka.
F. MAMBO YA KUFANYA ILI UWE NA MACHO YA KIROHO
i. Soma neno la Mungu
"Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia zangu" (Zaburi 119:105).
Neno la Mungu ni mwangaza. Linakumulikia pale usipoweza kuona kwa macho ya kawaida. Unaposoma neno la Mungu mara kwa mara inakupa wewe nafasi ya kujua siri za Mungu. Na huko ndiko kuona kwenyewe, maana siri za Mungu ziko kwenye ulimwengu wa roho. Na ili uzione inahitaji macho ya kiroho.
ii. Muombe Mungu akufumbue macho ya kiroho (Zaburi 119:18)
"Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako" (Zaburi 119:18)
Macho ya kiroho yanaweza kuzibwa. Kwahiyo unahitaji kumuomba Mungu, mtalamu wa kuzibua macho yako uweze kuona ya ulimwengu wa Roho. Bila huyo hakuna mwingine wa kukufumbua macho ya kiroho.
iii. Liishi neno la Mungu na maagizo yake (Zaburi 19:8)
"Maagizo ya BWANA ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya BWANA ni safi, Huyatia macho nuru (Zaburi 19:8). Kumbe unapoishi kwa kufuata maagizo na amri za Mungu (ambalo ni neno lake) unayapa macho yako ya rohoni uwezo wa kuona
iv. Pata dawa ya kutakasa macho kwa BWANA.
BWANA Mungu anayo dawa ya kutakasa macho ya kiroho na yakawa na uwezo wa kuona kila kitu. Wewe kazana kumuomba ili ayatakase yawe safi yaanze kuona vyema. Anasema hivi;
"Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona" (Ufu 3:18)
v. Acha kuwaza mabaya, badala yake tafakari mambo mema muda wote.
Ili macho yako ya kiroho yaanze kuona unatakiwa muda mwingi ubaki ukitafakari yaliyo mema. Usishiriki kutazama mambo maovu, kataa kutazama uharibifu. Biblia inasema;
"Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo" (Wafilipi 4:8)
Wako katika utumishi;
Frank Mwakapeta
+255 762 465 400

Comments
Post a Comment