THAMANI YA KITU ULICHO NACHO
KAMA HUONI THAMANI YA ULICHO NACHO, WENZAKO WANAKITAMANI
Kuna watu wana vitu vyenye thamani lakini wanavichezea tu. Hawajui kwamba kuna wengine wanavitamani. Wanatamani vingekuwa vya kwao.
Jaribu kufikiri kuhusu nguo. Je, umewahi kununua ama kununuliwa nguo mpya? Angalia jinsi ambavyo nguo mpya inakufanya uanze kudharau nguo zingine zile za zamani. Yawezekana kabisa kuna nguo ulikuwa unaipenda sana kabla hujanunua hii mpya. Lakini mara tu baada ya kununua mpya sasa hivi unaidharau ile ya kwanza, huoni thamani yake. Laiti ungejua kwamba kuna wengine wanatamani hata ile ya zamani waivae hakika usingethubutu hata kidogo kuidharau ile ya kwanza.
MAANA YA NENO "THAMANI"
Kamusi ya Kiswahili sanifu iliyoandikwa na TUKI na kuchapwa na Oxford, toleo la tatu, inatoa maana ya neno Thamani kuwa ni "Gharama au ubora wa kitu kutokana na hali ya kuhitajika kwake kwenye jamii". Wengine husema "Thamani ni ubora wa kitu kutokana na hali yake na umuhimu wake".
Yesu anasema;
Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako (Ufunuo 3:11)
Yesu kupitia mstari huu anataka kila mtu atunze kitu chake chochote cha thamani alicho nacho maana asipokitunza atakuwa amepoteza taji (ushindi, baraka, neema, kibali n.k). Yesu kufikia kiwango cha kuongea maneno haya ujue kabisa kwamba anatufahamu tunavyodharau vitu vyetu tulivyonavyo na kumbe ndivyo vyenye thamani. Kwa maana hii, unaweza ukawa unadharau kitu au jambo lako fulani kumbe ndilo la kukutoa kimaisha, ndilo la kukuweka mahali pazuri ama ndilo la kukufikisha mbinguni.
Kuna vitu vingi vya thamani ambavyo watu huona ni vya kawaida kiasi cha kuvidharau na kuvipuuza. Mfano wake ni;
1. Thamani ya sehemu zako za siri
2. Thamani ya kuwa Mkristo
3. Thamani ya wokovu (kuokoka)
4. Thamani ya kuwa mwanafunzi
5. Thamani ya Biashara/ofisi/kazi/ajira uliyonayo
6. Thamani ya ibada n.k
THAMANI YA KUWA MKRISTO
Mkristo ni nani?
Neno "Mkristo" limetumika mara tatu katika agano jipya (Matendo 11:26; Matendo 26:28; 1Petro 4:16). Wafuasi wa Yesu Kristo waliitwa kwa mara ya kwanza “wakristo” kule Antiokia (Matendo 11:26) kwa sababu tabia zao, matendo yao na hotuba zao zilikuwa kama za Kristo. Tunaweza kusema watu hawa walikuwa kama Yesu, walikuwa wa Kristo, walimilikiwa na Kristo kutokana na mienendo yao kufanana ya Yesu Kristo.
Mtu akiwa na uraia wa Tanzania anaitwa "M-Tanzania". Raia wa Kenya anaitwa "M-Kenya". Kumbe tunaweza kusema mtu wa Yesu Kristo anaitwa "M-Kristo". Kumbe kuitwa Mkristo ni jambo jema na ni tunu ya pekee. Hii ni kwa sababu unapoitwa Mkristo unakuwa chini ya uangalizi wa Kristo mwenyewe. Rais wa nchi anahakikisha anawahudumia wananchi maji, umeme, barabara na ujenzi wa zahanati. Anafanya hivyo kwa sababu ni wa kwake. Ndivyo inavyokuwa kwako mbele za Yesu; ukiitwa M-Kristo, atahakikisha anakupa kila hitaji kwa sababu wewe ni wa kwake (M-Kristo).
Wakati wewe unadharau ukristo ulionao kuna watu (ambao neema ya Kristo haijawazukia) wanatamani sana wangeitwa Wakristo. Wakati wewe unauchukulia Ukristo kama kitu cha kawaida tu, wenzako wanautumia kubadilisha maisha yao, uchumi wao, afya zao na ndoto zao.
Hivi unafahamu kwamba kuna watu wanatamani japo waitwe MAKRSITO (yaani wakristo bandia/ fake christians) ili tu angalau wawe na ka-harufu ka Ukristo? Kwanini wanafanya hivyo? Ni kwa sababu wanajua kuitwa Mkristo ni dili. Kwa namna gani kuitwa Mkristo ni dili kwa wapagani? Ni kwasababu akiitwa mkristo; kwanza, watu watamwamini. Wanaweza hata kumkopesha hela, kwa sababu wanajua Mkristo ni mwaminifu.
Yesu aliwatahadharisha wanafunzi wake kwamba;
Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. (Mathayo 24:24).
Ukiusoma kwa umakini mstari wa hapo juu utagundua kwamba kuna watu sio Wakristo ila wanatamani waitwe Wakrsito. Kwa nini? Kwa sababu sasa wamejua kuwa kuitwa Mkristo ni faida/dili (deal). Kwahiyo wako tayari waitwe japo kwa siku mbili tu ili wautumie vizuri. Sasa jaribu kufikiria kwamba wenzako wanaona bora hata waitwe MAKRISTO, lakini wewe uliye MKRISTO (wa Kristo) unadharau Ukristo. Huko ni kukosa akili.
Jaribu kufikiri itokee siku moja Rais amekuja mtaani kwenu halafu akawachagua watu watatu akae na kula pamoja nao. Jifanye wewe sio miongoni mwao, hujachaguliwa. Halafu fikiria kwamba mmoja wa wale watatu akatae kula na kupiga stori na Rais. Utamwonaje? Ninaamini utajisemea maneno mengi sana. Utasema "Ah! Hivi huyu ana akili kweli? Anakataa kukaa pamoja na Rais? Anachezea bahati!". Ndivyo ilivyo na kwako pia, watu wanakushangaa unapodharau ukristo wako. Wanaona unachezea bahati.
Nilipata kusimuliwa kwamba kulikuwa na kijana fulani aliyekuwa mpagani kabisa. Ikatokea amempenda binti fulani aliyekuwa ameokoka na akataka amuoe. Na alijua kabisa kwamba ili ampate, anapaswa kuanza kusali. Basi yule kijana ghafula akaanza kusali siku si nyingi akatangaza kuokoka na kuanza kuhudhuria ibada za walokole. Akaanza kumtongoza yule binti na binti alimkubalia kwa sababu naye aliamini kwamba tayari kijana kaokoka kama yeye. Mwishowe wakaoana. Baada ya kuoa, haikupita miezi mingi kijana akaacha kabisa kwenda ibadani.
Umeelewa hapo? Huyu kijana alikuwa mpagani na aligundua kwamba haikuwa rahisi kukubaliwa na wasichana bila kuwa Mkristo. Alichofanya ni kujifanya Mkristo ili aaminike. Na kweli aliaminika na kupata mke. Sasa kama MAKRISTO (Wakristo bandia) wanapata mke kwa sababu tu ya kujiita Mkristo, basi itakuwa zaidi sana kwako wewe uliye Mkristo wa kweli. Itakuwa rahisi sana kwako kuaminiwa na benki kubwa, mashirika makubwa, taasisi kubwa, viongozi wakubwa, makampuni. Itakuwa rahisi kwako Mkristo wa kweli kupata kazi, kuaminiwa kazini, kupata kibali kazini na mbele za watu.
Mpendwa mkristo, usipoona faida ya kuwa Mkristo, jaribu uwe mpagani japo kwa wiki moja uone jinsi utakavyokuwa unatutamani sisi uliotuacha kwenye ukristo wetu. Utaona wapagani (utakaoungana nao) jinsi wanavyotamani kuwa Wakristo. Watakwambia jinsi wanavyokabwa na wachawi usiku.
THAMANI YA WOKOVU/KUOKOKA
Watu wengi wanakataa kuokoka na hawaoni thamani ya Wokovu kwa sababu hawajui maana ya neno OKOKA. Kama wangejua, wasingekataa. KUOKOKA ni kunusurika. Kunusurika ni kuponea chupuchupu kwenye hatari ama jambo baya fulani. Ni kutoka kwenye eneo hatari na kwenda eneo lililo salama. Kwahiyo kuokoka ni kutolewa kwenye mikono hatari ya shetani na kuletwa kwa Yesu mahali salama.
Mtu akiokoka maana yake ameondokana na mateso ya shetani kama vile kurogwa, kufinywa na wachawi usiku, kutupiwa magonjwa na majini. Mtu akiokoka maana yake ameondoka kwenye mikono ya laana na mikosi ya shetani na kuingia kwenye ufalme wa Mungu wenye baraka tele tele. Zaidi sana, mtu akiokoka anakuwa na uhakika wa kuurithi ufalme wa Mungu. Sasa jambo kama hili sio la kulipuuza. Ni jambo la kulithamini sana, wokovu ni kitu cha thamani.
Ajabu ni kwamba, wapo wale ambao tayari wameokoka lakini wanauona wokovu kuwa si kitu kwao. Wanaona Wokovu ni kitu cha kawaida sana. Laiti wangejua kwamba kuna watu wanatamani waokoke kama wao, hakika wasingeudharau wokovu walio nao. Kuna watu wanatamani waokoke ili wasifinywe na wachawi tena, ila wamefungwa na shetani anayewazuia kuokoka.
Wakati wewe unaudharau wokovu ulio nao, kuna mwingine anatamani aokoke ili asiote tena ndoto za ajabu usiku. Wakati wewe unaudharau wokovu ulio nao, kuna mtu anatamani angekuwa wewe ili aweze kukemea mapepo yanayomtesa kila siku. Wakati wewe unasema wokovu ni hasara, kuna mwingine anaomba kabisa akisema; "Wokovu wako nimeungoja, Ee Bwana" (Mwanzo 49:18).
Mpendwa uliyeokoka, wokovu ulionao ni kitu cha thamani, ni lulu, ni madini. Uthamini, usiudharau.
THAMANI YA KUWA MWANAFUNZI (THAMANI YA ELIMU)
Kuna watu wengi walio mtaani aidha walifeli au hawakusoma kabisa, wanaotamani sana wangepata nafasi ya kusoma. Kuna watu walifanya fujo masomoni wakafukuzwa, na sasa wanajutia na wanatamani wangepewa nafasi tena ya kusoma. Kuna watu wameanzisha biashara lakini hawana elimu nazo namna ya kuziendesha, kwahiyo zinakufa. Wanatamani umri wao urudi nyuma warudi darasani lakini haiwezekani.
Laiti mwanafunzi angejua thamani ya kuitwa mwanafunzi, kamwe asingeichezea. Laiti angejua kwamba huko mtaani watu wanatamani warudi shule ili wapate maarifa, hakika angeacha uzembe bali angesoma kwa bidii. Kumbe Wakati wewe unadharau elimu, kuna wenzako wanatamani
Mungu naye anajua umuhimu wa elimu na anajua jinsi maisha yanavyokuwa magumu bila Elimu. Ndiyo maana anamsisitiza mwanafunzi akisema; "Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako" (Mith 4:13).
Sasa kama Mungu mwenyewe anasisitiza watu wasome wawe na elimu ya kutosha, kwanini watu wakatae kusoma? Kwanini watu watoroke shule? Yote hii ni kwa sababu watu hao hawajui thamani ya elimu na thamani ya kuwa mwanafunzi. Kama wanafunzi wangejua kuwa kuitwa mwanafunzi ni kitu cha thamani, wasingechezacheza shuleni, bali wangesoma kwa bidii ili wasije wakajuta pindi watakapoenda mtaani. Laiti wangejua kwamba mtaani ni kugumu bila kuwa na elimu, hakika wasingecheza-cheza shuleni
Kama wewe ni mzazi au mlezi, nisaidie kumwambia kijana ama binti yako maneno yafuatayo.
"Mwandishi wa somo hili ndugu Mwakapeta anasema nikuambie hivi; "kama wewe unaona elimu tukupayo haina maana, kuna wenzako wanatamani wangekuwa na wazazi wenye uwezo wa kuwasomesha ili nao wapate Elimu" .
PETRO ALIJUA THAMANI YA KITU ALICHOKUWA NACHO (MDO 3:1-8).
Kabla hatujaendea, hebu chukua Biblia usome Matendo ya Mitume 3:1-8. Baada ya kusoma, sasa tuendelee na somo. Tunaona kwamba Petro alitambua thamani ya kile alichokuwa nacho. Petro aliombwa pesa na yule kiwete, lakini Petro hakuwa na hela wala dhahabu. Alipotafakari akagundua kwamba licha ya kutokuwa na hela, bado alikuwa na kitu kimoja kikubwa sana kuliko hata pesa, na kitu hicho ni JINA LA YESU.
Akagundua kwamba jina la Yesu alilonalo lingeweza kuleta msaada mkubwa kwa kiwete zaidi ya zile pesa alizozitaka. Kwahiyo Petro akasema mimi sina pesa lakini nina kitu kimoja cha thamani nacho ni Jina la Yesu. Akamwambia Kiwete, kwa jina la Yesu simama uende. Yule mtu akasimama akaanza kutembea.
Watu wengi wanadharau kitu walichonacho. Kwa mfano watu wengi wanamwamini Yesu, lakini wanadharau nguvu ya huyo Yesu. Kwahiyo wanasali, wameokoka, wanamsifu, wanamwabudu, lakini wanashindwa kuliweka jina lake kwenye utendaji. Wanaamini kwamba jina la Yesu linaponya, lakini hawawezi kuliitia jina hilo kwa wagonjwa; wanabaki wanashangaa-shangaa tu.
Mtu yeyote anayemwamini Yesu ajue kabisa kapata kitu cha thamani na anapaswa kukithamini. Wala asikione ni cha kawaida. Wakati yeye anadharau, kuna wengine wanatamani wangemjua Yesu kama yeye amjuavyo. Laiti ungejua kwamba kuna watu wanamtamani Yesu uliye naye, hakika usingemchezea bali ungemtumia vizuri sana. Kama huoni thamani ya kuwa na jina la Yesu, kuna mwenzako anatamani.
TOWASHI ALITAMANI KITU ALICHOKUWA NACHO FILIPO
Ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume 8:26-38 utagundua kwamba Filipo na wenzake walikuwa wamerudi Yerusalemu baada ya kuhubiri injili ya Yesu maeneo mbalimbali. Ndipo Mungu akamwambia Filipo aende sehemu fulani. Na alipofika huko akamkuta mtu mmoja towashi, akisoma kitabu cha Isaya pasipo kukielewa. Filipo akamuuliza yule Towashi, "je, unayaelewa maandiko hayo?" lakini yule towashi akajibu akasema "nitaelewaje nisipokuwa na mtu wa kunielewesha?". Ndipo Filipo akaanza kumuelewesha. Baada ya kuelewa, akatamani abatizwe. Filipo akambatiza. Yule Towashi alirudi nyumbani kwake mwenye furaha kuu.
Katika habari hii tunaona mambo yafuatayo:
A. Filipo aliyajua maandiko lakini Towashi hakuyajua maandiko na ndiyo maana alimuomba Filipo amueleweshe. Wakati wewe unakaa tu bila kuwafundisha watu maandiko, kuna watu wanatamani wangepata mtu wa kuwafundisha neno la Mungu angalau kila jioni baada ya kazi. Wakati wewe unaona kuyajua maandiko si kitu, kuna watu wanatamani wangeyajua maandiko kama wewe. Amka sasa, anza kufundisha/kuhubiri neno maana kuna watu kama yule towashi wanahitaji mafundisho. Ukuyajua maandiko basi wewe una kitu cha thamani sana.
B. Towashi hakubatizwa hapo mwanzoni. Ndiyo maana aliomba abatizwe na Filipo kwa sababu alijua umuhimu wa kubatizwa. Wakati wewe unaona ubatizo ni kitu cha kawaida tu, kuna watu wanauona ubatizo kuwa kitu cha thamani na wanatamani wangebatizwa. Acha kudharau ubatizo wako, maana ubatizo ni kupokea uwezo wa roho mtakatifu.
ESAU HAKUJUA THAMANI YA KITU ALICHOKUWA NACHO
Biblia kwenye kitabu cha Mwanzo 25: 31-33 inasomeka hivi:
"Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza" .
Esau na Yakobo ni watoto wa baba mmoja, Isaka. Esau alikuwa mzaliwa wa kwanza na Yakobo alikuwa mdogo. Siku moja Esau alitoka kwenda kuwinda lakini hakupata kitu. Akarudi akiwa na njaa. Nyumbani alimkuta mdogo wake Yakobo. Na Yakobo alikuwa amepika supu ya Dengu. Basi ilibidi Esau aombe supu kwa mdogo wake. Mdogo wake akasema sawa nakupa lakini lazima uniuzie hicho cheo cha uzaliwa wa kwanza.
Yakobo alitamani sana cheo cha kaka yake cha kuitwa mzaliwa wa kwanza kwasababu alijua kabisa akiiitwa tu hivyo, baraka zote zitamwendea. Lakini Esau akadharau akasema ah! Kwani cheo cha uzaliwa wa kwanza kitanisaidia nini? Isitoshe nakaribia kufa. Akakubali kumpa mdogo wake uzaliwa wa kwanza. Yakobo akafurahi na akampa chakula. Esau alikubali kupoteza cheo na heshima eti kwa sababu tu ya njaa ya mlo mmoja.
Maamuzi haya yalimtesa Esau na kumfanya awe chini ya mdogo wake. Tunaona baadaye baba yao anambariki Yakobo kama mzaliwa wa kwanza, lakini Esau anaambiwa atakuwa mtumwa wa mdogo wake. Ni kweli baada ya kunenewa hayo na baba yake, tunaona ESAU anakuwa maskini lakini Yakobo anakuwa tajiri. Yakobo akawa na mali nyingi kuliko Esau. Hii ni sababu Esau alidharau thamani ya kitu alichokuwa nacho (Uzaliwa wa kwanza).
Je, umewahi kusikia watu wakiomba wakisema "ee Mungu wa Esau"? Mimi sikumbuki na kama wapo basi ni wachache. Lakini wengi wanaomba wakisema "Ee Mungu wa Yakobo". Wanamtaja Yakobo badala ya Esau ambaye alipaswa ndiye awe maarufu kuliko Yakobo. Lakini kwakuwa alidharau uzaliwa wa kwanza, ambao ungempa heshima hata kwa waombaji, ndio maana wala hatumtaji. Ukidharau ulicho nacho utapoteza heshima.
YUSUFU ALIJUA THAMANI YA KITU ALICHOKUWA NACHO
Ni kitu gani hicho? Alikuwa na vitu vingi vya thamani ambavyo tutaviangalia ndani ya somo hili. Kabla hatujaona thamani aliyokuwa nayo, hebu tumfahamu Yusufu ni nani. Yusufu ni mtoto wa mzee Yakobo. Alipendwa sana na baba yake. Hicho kilimfanya achukiwe sana na kaka zake kwa sababu baba yao alimpenda sana yeye kuliko wao. Maandiko yanaeleza kwamba kwa sababu ya kuchukiwa, Yusufu aliuzwa na kaka zake kwa watu wa Midiani. Wamidiani/Waishimaeli walijihusisha na biashara ya kununua na kuuza watumwa. Hao wakamuuza kwa Potifa, aliyekuwa akida na kiongozi wa kikosi cha Farao, mfalme wa Misri, kama maandiko yasemavyo;
"Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko".(Mwanzo 39:1).
A. Yusufu alisababisha baraka kwenye nyumba ya Potifa.
Akiwa nyumbani kwa Potifa, Yusufu akapata neema machoni pa Potifa, akapewa cheo kuwa mkuu/msimamizi wa kila kitu na vyote vilivyokuwa chini ya Potifa. Baada ya kumweka Yusufu kuwa mkuu wa vyote, ghafula Potifa akaanza kuona baraka tele. Mungu alimbariki Potifa kwa ajili ya Yusufu (Mwanzo 39:4,5). Hapa pana jambo la kujifunza; yaani kule tu kuishi na Yusufu, Potifa akawa anabarikiwa. Aisee kuna watu ambao uwepo wao ni baraka. Akiondoka tu na baraka zinaondoka. Wakati Yusufu anahisi kama anaongeza gharama za chakula nyumbani kwa Potifa, yeye Potifa anasema "nipate wapi mtu kama huyu mwenye kuniletea mibaraka nyumbani kwangu!" Wakati unajidharau kwa kitu ulicho nacho, kuna mtu anakitamani.
Huenda Yusufu alijiona wa kawaida tu lakini kumbe kuna watu walikuwa wanatamani thamani yake aliyokuwa nayo. Kwa upande mwingine, huenda Potifa na ndugu zake walimwona Yusufu kuwa kijana wa kawaida kawaida tu, lakini huenda majirani walikuwa wanasema kimoyo moyo; "aisee natamani ningeishi na Yusufu japo mwaka mmoja tu ili na mimi nibarikiwe kama Potifa". Ninaamini kabisa kama majirani wa Potifa wangejua kwamba baraka za Potifa zinatokana na uwepo wa Yusufu nyumbani mwake, hakika wangetamani hata wawe wanamkodi Yusufu kwa wiki, anakaa kwao kidogo kisha anarudi kwa Potifa; maana alibeba baraka.
Tunachojifunza;-
- Tufanyike baraka popote tunapokuwa
Kila alikoenda Yusufu walimtani. Wamidiani walimtamani wakaona anafaa kununuliwa awe mtumwa (anauzika). Potifa alimtamani akaona anafaa kuwa kiongozi wa Misri yote. Hebu na sisi tujitahidi kufanyika baraka kila mahali. Tabia na mwenendo wako ufanyike baraka uwapo shuleni, kanisani, sokoni na kwingineko. Muombe Mungu akufanye chanzo cha baraka popote unapokuwa. Ukiingia nyumba inayosumbuliwa na mapepo, wewe uwe sababu ya mapepo kukimbia, magonjwa kuondoka na laana kuondoka. Watu wasiseme "bora aondoke tu tumemchoka!"
- Kamwe tusijidharau.
Sisi tumebeba vitu vya thamani ndani yetu, ambavyo watu wakiviona wanatamani vingekuwa vyao.Watumishi wa Mungu hawapaswi kujidharau, badala yake wajue thamani yao. Ya kwamba wao wanaweza kutamka neno na likatoea. Wajifunze kuitamkia baraka miji wanamozunguka kwenye huduma. Kwa kuikanyaga miji na kutamka kwao , watakuwa wameleta baraka kwenye miji hiyo. Mfanyakazi wa ndani (House girl/boy) naye asijidharau. Amebeba kitu cha thamani. Asiseme mimi ni wa kufagia tu, bali ajue kwamba bila yeye kupika familia ya boss italala njaa. Bila yeye, nyumba itakuwa chafu, vyombo vitakuwa vichafu, watoto wa boss hawataenda shule. Kumbe yeye ni mtu muhimu sana. Ana kitu cha thamani sana.
B. Yusufu alijua thamani ya sehemu zake za siri, akakataa kulala na mke wa Potifa
Watu wengi hawajui kwamba sehemu zao za siri ni za thamani; wanaziachia hovyo kwa watu ambao sio waume/wake zao. Mpendwa msomaji; fahamu ya kwamba kitu chochote cha thamani kinahifadhiwa vizuri; hakiachwi nje nje hovyo, sio kila mtu anakiona, hapana. Ndiyo maana hata wewe hujawahi kuacha pesa nje ya nyumba, bali unaitunza ndani mahali salama. Kwanini unafanya hivyo? Ni kwa sababu pesa ni kitu cha thamani. Ndivyo ilivyo na kwa sehemu zako za siri; ni kitu cha thamani; sio kila mtu anapaswa kukiona, ni wewe tu labda na mke au mume wako (wa Ndoa), na sio kimada, danga wala mchumba
Sasa tuendelee. Biblia inatuambia kwamba Yusufu alikuwa mzuri wa uso. Basi mke wa Potifa alianza kumtamani Yusufu akitaka alale naye. Lakini Yusufu alikataa kabisa. Yule mama alizidi kumbembeleza siku hadi siku, lakini Yusufu bado alizidi kukataa, akasema asingeweza kutenda uovu ule hata amkosee Mungu (Mwanzo 39:9). Ndipo siku moja Yusufu akiwa ndani, yeye na mke wa Potifa (Maana Potifa hakuwepo siku hiyo), mke wa Potifa alimshika Yusufu akataka kumlazimisha alale naye, lakini Yusufu alikimbia (Mwanzo 39: 11, 12).
Kwanini Yusufu alikataa kulala na mke wa Bosi?
Ni kwa sababu aliijua thamani ya sehemu zake za siri. Alijua kabisa kwamba;
1. Kiungo cha siri sio cha kushikwa shikwa na kila mtu. Hapana
2. Alijua kabisa kwamba kufanya kitendo hicho kwa mwanamke ambaye hajamuoa ni dhambi.
3. Kiungo cha uzazi/siri hakipaswi kutumiwa kwa mtu ambaye sio mke wala mume wa ndoa. Ni kwa ajili ya mke au mume wa ndoa tu, baaasi.
4. Kiungo cha uzazi sio cha kushikwashikwa na michepuko.
5. Alijua kwamba bado hajaoa, kwahiyo haruhusiwi kufanya ujinga kwa kutumia kiungo chake cha uzazi/siri.
6. Alielewa kabisa kwamba kwa kufanya vile kungeweza kumletea magonjwa ya zinaa.
7. Alitambua kabisa kwamba kiungo chake cha uzazi (siri) kimebeba familia yake ya baadaye (watoto). Kwahiyo akichezea, anaharibu hazina ya hapo baadaye.
Tunachojifunza;-
Wakati wewe unaachia-achia hovyo kiungo chako kwa wasichana/wavulana, mwenzako Yusufu alikataa; maana alijua thamani ya kiungo hicho, ya kwamba sio cha kuchezewa
Wakati wewe unasema hakuna haja ya kukihifadhi hicho kiungo, wapo wavulana/wasichana wanaokutamani wakiguse kiungo chako hicho ili wachukue thamani iliyomo ndani ya kiungo chako hicho.
Wakati wewe uliyejitunza (uliye bikira) unasema hakuna sababu ya kutunza ubikira wako, wapo waliopoteza kizembe na wanatamani wangekuwa kama wewe wangejitunza.
MUNGU HUTUMIA KILE ULICHO NACHO KUFANYA KAZI YAKE PAMOJA NAWE
Kwa lugha nyepesi naweza kusema, Mungu hawezi kumtumia mtu asiye na kitu. Jiulize una nini ili Mungu akutumie. Ikiwa una kitu, basi anapotaka kukutumia kama mtumishi wake hawezi kufanya lolote kupitia wewe ikiwa wewe mwenyewe hutatumia kile ulicho nacho. Ananyamaza mpaka pale wewe mwenyewe utakapoona thamani ya kitu ulicho nacho na kuamua kukitumia. Hapo ndipo naye hushuka na kufanya jambo ulilotaka.
Kwa mfano unataka Mungu amponye mgonjwa fulani; hapo Mungu ataangalia je una nini kitakachomshawishi amponye yule mgonjwa? Je, una imani kuhusu Mungu? Una nini? Hicho ndicho Mungu hutumia kutenda ulilomuomba.
Hebu tuwaangalie watumishi kwenye Biblia jinsi walivyotumia kile walichokuwa nacho kufanya kazi ya Mungu pamoja naye.
1. PETRO NA JINA LA YESU
Utakumbuka kisa cha Petro na Yohana kwenda hekaluni kusali, na kwamba walipofika wakamuona mtu kiwete tangu kuzaliwa akiombaomba watu wamsaidie (Matendo ya mitume 3:1-8). Ndipo wakaenda kumuombea kwa JINA LA YESU akainuka na kuanza kutembea.
Ajabu ni kwamba siku zote Mungu alimuona yule kiwete lakini hakumponya. Mungu alinyamaza bila kuponya kwa sababu alitaka Petro na Yohana wajifunze kutumia kitu walicho nacho (jina la Yesu) kumfanya Mungu atende kazi pamoja nao. Hata Petro na Yohana walikuwa kila siku wanaenda hekaluni na walikuwa wanamuona kiwete lakini wasimponye. Kwanini? Ni kwa sababu awali hawakujua thamani ya kitu walichokuwa nacho (jina la Yesu) kinavyoweza kumvuta Mungu kuja kumponya kiwete. Siku walipoamua kutumia kitu walicho nacho (waliposema kwa jina la Yesu simama uende), ndipo Mungu akashuka kumponya kiwete.
Kumbe yawezekana watu wengi wamefungwa na shetani si kwamba Mungu hawaoni; anawaona lakini anasubiri sisi watumishi wake tutumie tulivyo navyo ndipo awafungue. Tuna vitu vingi vya thamani kama vile Jina na damu ya Yesu, ambavyo kama tutavitumia, basi Mungu atashuka kuwafungua. Lakini tukinyamaza bila kuwatamkia kwamba "kwa jina la Yesu funguka", na Mungu pia atakaa kimya bila kuwafungua.
2. MUSA NA FIMBO YAKE
Mungu alitumia kitu alichokuwa nacho Musa kutenda kazi pamoja na Musa na kuudhihirisha ukuu wake. Musa alikuwa na nini? Alikuwa na fimbo. Mungu alipotaka kuwaokoa wana Israeli mikononi mwa Farao, aliamua kumtuma Musa. Lakini Musa alikuwa mwoga na mwenye hofu. Mungu akawaza namna ya kumfanya Musa aende Misri.
Ndipo "Bwana akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo" (Kutoka 4:2). Musa alipojibu, Mungu akamwambia nitatumia fimbo yako kuwaokoa watu wangu wa Israeli. Wewe nenda tu, ukifika kwa farao dondosha hiyo fimbo chini, itageuka kuwa nyoka. Hapo Farao atajua kwamba ni mimi Mungu nimekutuma na atakuruhusu uwachukue watu wangu Israeli. (Kutoka 4:3-5).
Mungu hawezi kumtumia mtu asiye na kitu. Jiulize mwenyewe una nini ili Mungu akutumie kutangaza ufalme wake.
Je, ni mwimbaji akutumie kutangaza neno lake kwa kuimba?
Je, ni mwombaji akutumie kuombea wwnye shida?
Je, una neno la Mungu ili akutumie kuhubiri watu?
Je, una misuli ili Mungu akutumie kubeba wanaolipuka mapepo kwenye mikutano?
Una nini?
Je, una hela ili Mungu akutumie kwa pesa zako kujenga makanisa, kusaidia wahitaji na kusaidia huduma mbalimbali?
MUNGU HUTUMIA ULICHO NACHO KUKUBARIKI
Ili Mungu akubariki anatafuta pa kuanzia ili aachilie hizo baraka kwako. Je, una nini ili Mungu atumie hicho kukubariki? Sasa ukisema huna chochote unampa Mungu shida aanzie wapi kukubariki.
Sawa huna mtaji mkubwa, lakini je, huna hata elfu kumi ufungue genge ili Mungu aanzie hapo kukubariki?
Ni kweli hujasoma, lakini je, huna hata kipaji fulani ili Mungu atumie kipaji hicho kukubariki?
Najua huna hela, lakini je, huna hata ardhi ya kulima ili Mungu akubariki kupitia kilimo chako?
Una nini sasa ili Mungu aanzie hapo kukubariki?
Wenzako kwenye Biblia walikuwa wanathamini kitu kidogo walichokuwa nacho, na Mungu alitumia kidogo hicho kuwabariki. Ndiyo maana nasema jifunze kuthamini kitu ulicho nacho. Hebu tuwaangalie watu wafuatao
A. Mama mjane alikuwa na chupa moja tu ya mafuta na Mungu akaitumia hiyo kumtajirisha/kumbariki
Huyu mama alifiwa na mumewe. Kabla hajafa alikuwa anadaiwa na watu wengi. Kwahiyo alipokufa, mke wake akabaki na mzigo wa madeni. Ghafula mmoja wa wale waliokuwa wanadai akamwendea yule mama akitaka kupewa mali yake. Na kwamba asipomlipa basi atawachukua watoto wa yule mama.
Yule mama akaamua kwenda kwa mtumishi Elisha kumueleza tatizo hilo huku akilia sana. Akamwambia "mtumishi, nimekuja kwako kwa sababu unajua kabisa mume wangu alikuwa mtumishi wako na alikuwa mcha Bwana, lakini anayemdai amekuja na anasema nisipomlipa atachukua wanangu wawili wawe watumwa wake" (Soma 2Wafalme 4:1).
Elisha aliposikia maneno ya yule mama, naamini alijisemesha moyoni kwamba "sasa huyu mama analialia nimsaidiaje? Siwezi kumsaidia kama hana kitu chochote ambacho mimi naweza kuanzia hapo kumsaidia". Ndipo Elisha aliamua kumuuliza yule mama, akasema;
Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta.
Umeona sasa! Kumbe huyu mama alikuwa na chupa ya mafuta lakini aliidharau. Hakuona thamani ya kitu alichokuwa nacho. Aliona kama ile chupa haiwezi kumsaidia kulipa madeni ya mume wake. Kwahiyo alibaki analia-lia tu. Kama angeona thamani ya ile chupa ya mafuta, asingelialia hovyo, maana huo ni mtaji tosha.
Elisha akamwambia, "Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge" (2Wafalme 4:3,4). Basi yule mama akafanya kama alivyoagizwa, akakusanya vyombo akajifungia yeye na watoto wake. Wakaanza kumimina mafuta kwenye vile vyombo, vikajaa vyote.
Baada ya kuvijaza vyombo vyote, alirudi kwa nabii Elisha kumjulisha kwamba tayari vyombo vyote vina mafuta. Elisha akamjibu akasema, "Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako."
Mpendwa msomaji, ni wazi kwamba chupa moja isingeweza kujaza vyombo vyote vya kabatini hadi vile alivyoazima kwa majirani, bali ulikuwa muujiza wa Mungu ili aweze kulipa madeni. Lakini amini kabisa kwamba kama yule mama asingekuwa na chochote, na Mungu naye asingemsaidia. Mungu alihitaji kuona chochote hata kama ni kidogo, ili aanzie hapo kumbariki yule mama.
B. Mjane wa Sarepta alikuwa na unga kidogo na mafuta kidogo, Mungu akavitumia kumbariki
Katika kitabu cha 1Wafalme 17:10-16 tunaambiwa kwamba nabii Eliya aliambiwa na Mungu aende mji wa Sarepta. Alipofika huko akamkuta mjane. Akamuomba amuandalie chakula (mkate) ale maana alikuwa na njaa. Yule mama akamjibu Eliya akasema, "sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe". (1Wafalme 17:12)
Kwa mstari huu tuliosoma inaonesha kabisa kwamba mama hakuwa na matumaini ya kuishi tena, maana alidharau kile alichokuwa nacho. Hakujua kwamba Mungu angeweza kumbariki kwa kutumia kile kichache alichokuwa nacho (unga kidogo na mafuta kidogo) na akaongezewa siku za kuishi.
Ajabu ni kwamba alipokubali kupika kwa ajili ya nabii, lile kapu lenye unga kidogo likawa na unga wa kutosha. Ile chupa ya mafuta haikuishiwa mafuta. Yule mama aliyedhani angekufa kwa sababu ya kukosa chakula hakufa; badala yake aliishi miaka mingi baadaye.
Kwahiyo tumeona kwamba ili Mungu ambariki mtu anaangalia je huyo mtu ana nini? Ana kitu gani ili nianzie hapo kumbariki? Huyu mama alikuwa na unga kidogo na mafuta kidogo, Mungu akavitumia hivyo hivyo kumuongeza unga wa kutosha, mafuta ya kutosha na miaka mingi ya kutosha. Ndivyo ilivyoandikwa katika 1Wafalme 17:16; "Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.
C. Hezekia alikuwa mkaminifu, mkweli na mtenda mema", Mungu akatumia hivyo kumuongeza miaka 15 ya kuishi
Tunasoma katika maandiko kwamba "Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii,...............akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona." (Isaya 38:1).
Hezekia alipoambiwa hayo, aliingia kuomba. "akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana." (Isaya 38:3).
Ninaamini Mungu aliposikia maombi ya Hezekia, aliwaza sana na kujiuliza kwamba 'Sasa huyu Hezekia anaomba nimsamehe, ana nini cha kunishawishi ili nimsamehe?'. Nadhani baadaye akatafakari na kusema "kwakuwa ana ukweli, ukamilifu na mtenda mema, basi nitamsamehe".
Ndipo Mungu akaamua kumtuma Isaya kwa Hezekia, akisema 'Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.'(Isaya 38:5).
Ule ukweli, ukamilifu na wema wa Hezekia ulimfanya asamehewe. Kile alichokuwa nacho ndicho kilimsaidia kupata msamaha.
UJUMBE KUTOKA KWENYE 2WAKORINTHO 4:3
Neno la Mungu limeandikwa hivi;
"Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu"
Paulo alifika mahali amehubiri vya kutoka kiasi kwamba kila mtu alitakiwa kuelewa. Sasa anasema "jamani kama kuna mtu hajaelewa injili hii niliyohubiri, basi ni yule tu ambaye mungu wa dunia (shetani) amempofusha ufahamu (fikira) ashindwe kuyaelewa mahubiri yangu".
Na mimi Frank Mwakapeta nasema hivi, Ikiwa somo hili limesitirika (yaani kama halijaeleweka) kwa mtu fulani hapa, basi ni kwa yule ambaye shetani amempofusha macho na akili ili asiweze kuona faida (Thamani) ya somo hili na thamani ya kile alicho nacho.
Shetani hapendi mtu afanikiwe. Akiona kuna mafundisho au neno linaloweza kumfungua mtu na kumfanya aweze kuona thamani ya mwili wake au nafasi yake; anamzuia mtu huyo asielewe neno hilo; ili aendelee kubaki gizani kwenye tabia mbaya, kwenye uchafu na kwenye hasara.
Anachokifanya shetani ili mtu asifanikiwe, ni kumpofusha macho. Yaani kumfanya asione thamani ya kile alicho nacho bali aone ki-vingine tu. Mfano;
1. Thamani ya wokovu/kuokoka. Wakati watu wengine wanatamani waokoke ili wasichezewe na wachawi na waweze kuurithi ufalme wa mbinguni, yule aliyeokoka atakuwa anaona wokovu si kitu. Shetani anampofusha macho asione faida ya kuokoka. Hataona kama wokovu ni kitu cha thamani
2. Thamani ya kuwa mwanafunzi. Wakati wale walio mtaani, waliokosa ada, waliokosa watu wa kuwasomesha wanapotamani wangekuwa shule, huyu ataona kama kusoma ni kupoteza muda. Ataona hakuna haja ya kuwashukuru wala kuwaombea wazazi wanaotafuta ada. Wakati binti aliyepata mimba shuleni anatamani kurudi shule, huyu ataona kama kusoma kunamnyima muda wa starehe na wavulana
3. Thamani ya kazi. Wakati wenzako wasio na kazi wanatamani wangepata ajira hata kama ni ndogo kuliko yako, wewe unaidharau na kuona haifai. Ni kwa sababu haujui thamani ya kitu ulicho nacho (hiyo ajira), shetani amepofusha macho yako usione thamani ya kazi hiyo
4. Thamani ya uhuru wa kuabudu. Wakati wenzako nchi zingine wanatamani waruhusiwe kwenda kanisani, wewe uliye na uhuru unadharau ibada. Ni kwa sababu huoni thamani ya kitu ulicho nacho. Na shetani amepofusha macho usione kitu kilicho chema.
5. Wakati wanafunzi wengine wanaona umuhimu wa kushiriki ibada yeye ataona ni kukwamisha ratiba zingine za masomo
6. Wakati wengine wanaona umuhimu wa kuwepo umeme shuleni, yeye ataona unamharibia ratiba ya kulala mapema.
7. Wakati wengine wanaona faida ya kusoma shule ambayo muda wote walimu wapo, yeye ataona kama ni kero, wanamkwamisha na kuzuia raha ya kusinzia darasani
8. Wakati wanafunzi wengine wanatamani wawe na walimu wanaowapa maswali mara kwa mara ili kuongeza ujuzi wa walichokisoma, yeye ataona kuwa na walimu wa namna hiyo ni kero
9. Wakati unaona genge la biashara ulilo nalo si kitu, kuna mwenzako hana hata mtaji wa kununulia machungwa kumi ili naye aanzishe biashara.
10. Wakati wewe unasema Tanzania ni nchi mbaya, kuna mtu yuko nchi yenye vita anatamani angeishi Tanzania mahali palipo na amani.
11. Wakati wewe unamsema vibaya mtoto/mume/mke wako kuwa hafai, kuna mtu anatamani angekuwa wa kwake, maana yeye hana hata wa aina yako
12. Wakati wenzako wasio na wazazi wanatamani wangekuwa na mzazi wamheshimu, Shetani atakupofusha macho atakufanya uwatukane wazazi wako na kuona si kitu
13. Wakati wenzako wanakataa kulala na mke au mume wa mtu, wewe utasema "Ah, wapi, kwani kuna shida gani, kwani kiungo kitakatika au kupungua saizi yake (size)?". Hapo ujue ni shetani amepofusha macho yako usione madhara ya uzinzi.
Mpendwa msomaji, kuanzia leo thamini ulicho nacho. Mungu akusaidie. Amina.
Wako katika utumishi;
Frank Mwakapeta
+255 762 465 400
Ubarikiwe na Mungu wa kweli
ReplyDelete